Hayo yametangazwa bayana na Mwendeshamashtaka mkuu wa taifa Valentin Bagorikunda na ni kufuatia mauaji ya watu 39 yaliyoendeshwa hapo ijumapili nyakati za saa mbili za usiku na watu wenye kubebelea silaha na kuvalia sare za kijeshi na za polisi dhidi ya kilabu huko Gatumba, ni kwenye umbali wa km 15 magharibi mwa mji wa Bujumbura.
Na kuundwa tume hio ni hasa kutokana na maagizo au uamzi wa Rais wa Jamhuri ya Burundi Pierre Nkurunziza wa kuvitaka vyombo vya sheria kuendesha, kwa muda usiozidi mwezi moja, uchunguzi juu ya mauaji hayo na kutowa mwanga ili waliohusika na vitendo hivyo viovu wafikishwe mbele ya mahakama na waadhibiwe vikali. « Ikiwa vitashindwa kutaitishwa vyombo vya sheria vya kimataifa’’, alisema hayo Rais wa Jamhuri, Pierre Nkurunziza ambae anatarajiwa kushiriki kikao kikuu cha Umoja wa Mataifa huko New York.
Tume hio ya uchunguzi juu ya mauaji ya Gatumba ni pamoja na maofisa 3 wa polisi na majaji 4, na halmashauri hio inaongozwa na Adolphe Manirakiza kutoka Mahakama kuu ya taifa. Mwendeshamashtaka mkuu wa taifa Valentin Bagorikunda ametahadhari vyombo vya habari au mashirika ya kiraia kua atakaethubutu kutowa habari au udadisi kuhusu taratibu za uendeshwaji uchunguzi huo ataadhibiwa kwa mujibu wa sheria.
’’Kuna ulazima uchunguzi huo ufanyike kwa makini bila mwingilio wa wanasiasa, wanaharakati wa haki za binadamu na wandishi habari ili ukweli usipotoshwe sababu kuna wale ambao wanaonekana kuchochea uhasama’’, alisema hayo waziri wa Burundi wa mambo ya ndani Edouard Nduwimana akisoma taarifa iliyotolewa hapo usiku wa kuamkia leo bada ya kikao cha Baraza kuu la Usalama chini Burundi. Na lengo lilikua ni kuchunguza hali ya usalama na hasa kutathmini mauaji hayo yailiyotokea huko Gatumba.
Hayo ni wakati baadhi ya mashirika ya haki za binadamu yakidai kusifanyike uchunguzi kuhusu mauaji hayo ya Gatumba tu, bali kuendeshwe uchunguzi juu ya mauaji yote yanayozidi kufanyika hapa na pale kote nchini. « Tunavihimiza vyombo vya dola hasa vyombo vya sheria kufanya uchunguzi kuhusu mauaji hayo yaliyofanyika huko Gatumba ili waliahusika na ukatili huo waadhibiwe na tunaviomba pia vyombo hivyo visipuuzie mauaji mengine yanayozidi kufanyika, hayo ni wakati maiti zikizidi kuokotwa hapa na pale », anasema hayo Pacifique Nininahazwe kiongozi wa muungano wa mashirika ya kiraia nchini Burundi, ’’FORSC’’.