Bada ya watu zaidi ya 39 kuuwawa na wengine zaidi ya 10 kujeruhiwa huko Gatumba (maghariba mwa mji wa Bujumbura) hapo ijumapili usiku katika shambulio dhidi ya kilabu lililoendeshwa na watu wenye kuvalia sare za kijeshi na za polisi na kubebelea silaha, Jumuia ya kimataifa, vyama vya siasa na mashirika ya kiraia yanazidi kulani mauaji hayo na yanaomba vyombo vya vianzishe uchunguzi ili waliohusika katika kitendo hicho waadhibiwe.
Serekali ya Burundi ilitoleya wito vyombo vya sheria ikivitaka kutoa mwanga kuhusu mauaji hayo katika muda usiozidi mwezi moja ili waliohusika katika kitendo hicho waadhibiwe na ’’ikiwa vitashindwa kutaitishwa vyombo vya sheria vya kimataifa’’, alisema hayo Rais wa Jamhuri, Pierre Nkurubnziza ambae amejielekeza huko New York kushiriki kikao kikuu cha Umoja wa Mataifa.
Kwa jumla vyama vya siasa nchini Burundi vinalani vikali mauaji hayo bila kusahau mashirika ya kiraia ambayo yanaomba walioendesha mauaji hayo ya kikatili waadhibiwa vikali. Mashirika hayo yanaomba pia kufanyike uchunguzi ili kutolewe mwanga kuhusu maiti zinazozidi kuokotwa hapa na pale.
Mashirika hayo ya kiraia ikiwa ni pomoja na APRODH, Ligue Iteka, OAG, FORSC na mengineyo yanahakikisha kua watu zaidi ya 100 waliuwawa tangu mwezi mei mwaka huu katika operesheni za kuwasaka wafuasi wa Agathon Rwasa kinara wa chama cha waasi cha zamani cha FNL. Wakati huu aliingia mafichoni bada ya madai ya uizi wa kura katika chaguzi za hapo mwaka jana zilizopelekea chama cha CNDD FDD kubuka ushindi.
Upande wa Jumuia ya kimataifa, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon analani vikali mauaji hayo ya Gatumba. Anasema wakati Burundi ikiwa mbioni katika harakati za kuboresha amani bada ya miaka zaidi ya 10 ikiwa katika lindi la machafuko, shambulio hilo halieleweki. Umoja wa Mataifa unaomba waliohusika katika vitendo hivyo waadhibiwe kwa mujibu wa sheria huku ukitolea wito pande zote ukizitaka kutoendelea kuzozana.
« Serekali ya Umarekani inalani na inasikitishwa na mauaji hayo dhidi ya mgahawa huko Gatumba ambayo yanaonekana kua yalikusudiwa », inasema taarifa kutoka kwenye ubalozi wa Umarekani jijini Bujumbura. Serekali ya Umarekani inayiomba serekali ya Burundi ifanye kila iliwezalo ili waliotenda unyama huo wafikishwe mbele ya mahakama. Serekali ya Umarekani inaziomba pande zote kukomesha mauaji na kudumisha maridhiano.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Ubelgiji, Steven Vanackere analani vikali mauaji hayo yaliyofanyika huko Gatumba katika mgahawa. Anasema kutiwa hofu na hali ya kuzuka tena machafuko nchini Burundi. « Kamwe vurugu si suluhisho kwa matatizo nchini Burundi », anazidi kusema Waziri huyo wa mambo ya kigeni wa Ubelgiji huku akiomba makundi ya wapiganaji kutia silaha chini. Waziri Vanackere anakiri kua mazungomzo ya kisiasa, maafikiano na kuliendeleza taifa bila ubaguzi kwa manufaa ya kila raia na chini ya uheshimishaji wa taasisi zilizoteuliwa na misingi ya kidemokrasi, ndio njia pekee ya kuyatanzua matatizo yanayoikabili Burundi.