Kwa mujibu wa duru za kuaminika, serekali ya mpito ya Somalia inabaini kua wapiganaji 6 wa kundi la Al-Shabaab waliuawa hapo alhamisi disemba 8 huko Karan na Huriwa kaskazini mwa mji wa Mogadishu katika mapigano kati ya wapiganaji hao na askari wa serekali ya mpito wanaoungwa mkono na vikosi vya Umoja wa Afrika. <doc2285|left>Mmoja kati ya wasemaji wa kundi hilo anakiri kua kuliuawa askari 9 wa serekali na wengine 4 kutoka vikosi vya Umoja wa Afrika katika mapigano hayo. Yote hayo yalianza nyakati za alfajiri bada ya askari wa serekali kushambuliwa na wapiganaji hao wa Al Shabaab. Ilibidi vikosi vya Umoja wa Afrika vilivyotumwa nchini humo kurejesha amani vitumie vifaru na zana nzito. Wachunguzi wa mambo wanabaini kua pengine wapiganaji wa Al-Shabaab wana nia ya kurejea kwenye ngome zao za zamani mjini Mogadishu. Hayo ni baada ya Al-Shabaab kuchukuwa uamzi wa kuondoka Mogadishu hapo mwezi ogasti na serikali kutangaza kuwa inaudhibiti mji huo. Na hapo ijuma tano wapiganaji wa Al-Shabaab walishambulia kambi ya kijeshi inayosimamiwa na vikosi vya Umoja wa Afrika katika mji wa Wadajir kusini mwa Mogadishu. Umoja wa Afrika una vikosi takriban 9,000 mjini Mogadishu vilivyotumwa nchini humo kurejesha amani na hasa kuunga mkono serikali ya mpito. Kenya pia imetuma askari wake kusini mwa Somalia tangu mwezi Octoba, kufuatia hujuma za wapiganaji wa Al Shabaab na utekaji nyara kwenye mpaka baina nchi hizo mbili. Bunge la Kenya liliisha kubali jeshi la Kenya lijiunge na vikosi vya Umoja wa Afrika nchini Somalia.