Kwa mujibu wa duru za kuaminika kutoka chama chake cha FRODEBU, Bw. Léonce Ngendakumana ambae pia ni kiongozi wa mungano wa vyama vya upinzani nchini Burundi, ADC-Ikibiri amekamatwa na askari polisi leo alfajiri na wakati huu anahojiwa mahakamani. Duru hizo zasema hata viongozi wengine wa chama hicho cha FRODEBU, wamepewa waranti na wanahojiwa mahakamani pia.
Wakati hayo yakiarifiwa duru zasema hata mwanaharakati wa haki za binadamu, Pierre Claver Mbonimpa, kiongozi wa shirika liitwalo ’’APRODH’’ amepewa waranti hapo usiku wa kuamkia leo na anatazamiwa kuhojiwa pia mahakamani.
Hayo ni bada ya kutangaza bayana kua kuna operesheni iitwayo ’’Safisha’’ambayo ni msako unaoendeshwa na polisi dhidi ya ’’makundi ya wajambazi na wafuasi wa Agathon Rwasa’’, kinara wa zamani wa chama cha waasi cha FNL aliyeamuwa kuingia mafichoni baada ya madai ya uizi wa kura katika uchaguzi wa hapo mwaka jana uliopelekea chama cha CNDD FDD kujinyakulia ushindi.
Si mara ya kwanza mwanaharakati huyo wa haki za binadamu nchini Burundi, kuiitishwa mahakamani kujieleza kuhusu operesheni hio na alibaini kua ’’operesheni hiyo na matamshi hayo si mambo aliyoyazua bali ni maneno kutoka kwa walionusurika katika msako huo unaoendeshwa na polisi. Kiongozi wa shirika hilo liitwalo ’’APRODH’’ anakiri kua ’’walionusurika wanabaini kua waliyasikia yakisemwa na askari polisi wakati wa msako huo ambao unafanyika kwa ushirikiano fika na vijana wakereketwa wa chama tawala cha CNDD FDD”. Madai hayo yanakanushwa na kutupiliwa mbali na kiongozi wa vijana hao, mbunge Ezéchiel Nibigira.