Kwa mujibu wa duru za kuaminika watu zaidi ya 39 wameuwawa wengine zaidi ya 10 wakajeruhiwa hapo usiku wa kuamkia leo nyakati za saa mbili huko Gatumbu, ni kwenye umbali wa km 15 magharibi mwa mji wa Bujumbura. Hayo yamefanyika katika shambulio la watu wenye kubebelea silaha dhidi ya kilabu kiitwacho ’’Les Amis’’.
Duru hizo zasema watu hao walikuwa wakivalia sare za kijeshi na za polisi, baadhi yao walikuwa na bunduki za rashasha. ’’Shambulio hilo lilidumu mda wa dakika 25 walakin ilikuwa ni moto wa jahanama’’, anasema mtu moja ambae amenusurika huku akiomboleza kifo cha mdogo wake.
Rais wa Jamhuri ya Burundi Pierre Nkurunziza ambae amejielekeza leo asubuhi huko Gatumba kushuhudia hali ya mambo bada ya shambulio hilo, ameamuru na kutangaza rasmi siku tatu za maombolezi ya Taifa kufuatia mauaji hayo ya kikatili.
Baadhi ya mawaziri pakiwemo waziri wa ulinzi na waziri wa usalama wa raia wamejielekeza huko Gatumba. Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao nchini Burundi na wanamemba wa Halmashahuri Huru ya Haki za Binadamu pamoja na wajumbe wa mashirika ya haki za binadamu pakiwemo Pacifique Nininahazwe, kiongozi wa Muungano wa mashirika ya kiraia, FORSC wamejielekeza pia huko Gatumba. Wote kwa ujumla wanalani mauaji hayo ya kikatili.
Rais Nkurunziza ameamba vyombo vya sheria vianzishe haraka iwezekanavyo uchunguzi ili walihusika katika kitendo hicho waadhibiwe vikali. Amebaini kua ikibidi serekali ya Burundi itaomba vyombo vya sheria vya kimataifa vichangie ili wahalifu hao wakamatwe. Musiba huo umesababisha Rais wa Jamhuri kuahirisha ziara yake huko New York kwenye makao ya Umoja wa Mataifa. Alikua akitazamiwa kushiriki kikao kuhusu haki za binadamu.
Mauaji ya kinyama…
« Ilikuwa ni karibu saa moja na dakika 40 watu, walikuwa wakitumia bia huku vijana wakipitapita na mishikaki, watoto, wanawake na watu wengine wakicheka na kucheza muziki, muda mdogo tukaona watu wenye kuvalia sare za polisi na za kijeshi. Papo hapo tulipatwa na uoga na kuanza kutangatanga walakin walikuwa wameisha anza kuripuwa maguruneti huku wengine wakifyatuwa risasi’’, amesema hayo mtu mwengine ambae amenusurika kwa sauti yenye huzuni. Wakati huu ni kibogoyo ameyapoteza meno mawili.
« Askari polisi wamewasili bada ya watu hao kuondoka huku wakiendelea kupiga risasi hewani. Kumehesabiwa papo hapo maiti 20 na wengine wanazidi kuiaga dunia katika hospitali na zahanati mbalimbali », amebaini hayo mkaazi wa kijiji hicho cha Gatumba akihakikisha kua shambulio hilo haliwezi kuambatanishwa na mambo ya kisiasa sababu ’’mwenye kilabu hicho ambae ameyapotea maisha katika shambulio hilo alikua haegemee upande wowote’’.
Duru zingine zasema pengine ni ulipizaji kisasi bada ya operesheni za kuwasaka wafuasi wa Agathon Rwasa, kinara wa chama cha zamani cha waasi cha FNL aliyeamua kuingia mafichoni bada ya madai ya uizi wa kura katika chaguzi za hapo mwaka jana zilizopelekea chama cha CNDD FDD kijinyakulia ushindi.