<doc1399|left>Ibada hio ilikuwa hasa ni katika sherehe za kutinda msiba, kando ya wakaazi wa mtaa wa Gatumba ibada hio ya misa ilihuduriwa na makamo wa pili wa rais Gervais Rufyikiri. Misa hio ilihudhuriwa pia na mawaziri wa serekali ya Burundi pakiwemo waziri wa ulinzi, waziri wa usalama wa raia, waziri wa mambo ya ndani, waziri wa mshikamano wa kitaifa, waziri anayehusika na maswala ya Jumuia ya Afrika Mashariki, waziri wa wafanyakazi wa serekali na msemaji wa serekali. Maseneta na wabunge walishiriki pia sherehe hizo za maombolezi. Katika ibada hizo kulionekana pia mabalozi, Rais wa zamani wa Burundi, Domitien Ndayizeye na mkewe na waakilishi wa mashirika ya kiraia pakiwemo mwanaharakati wa haki za binadamu Pierre Claver Mbonimpa, kiongozi wa shirika la APRODH.
Misa hio ilisomwa na Askofu Anatole Ruberinyange, licha ya kua picha kanisani ilikua haiwezi kufananishwa na ile ya majonzi ya hapo ijuma tatu wakati wa mazishi ya watu hao 39 waliouwawa kikatili, hali ilikuwa ni ya huzuni. Askofu Ruberinyange alisisitiza umuhimu wa mshikamano, umoja na kuheshimu uhai wa kila binadamu.
Katika risala yake makamo wa pili wa rais, Gervais Rufyikiri alikiri kua serekali ya Burundi italifanya kila iliwezalo ili waliohusika kwa njia moja au nyingine katika mauaji hayo ya Gatumba yaliyapelekea watu 39 kuuwawa wakamatwe, wafikishwe mahakamani na waadhibiwe kwa mujibu wa sheria.
Alivikumbusha vyombo vya habari amri iliyotolewa na serekali ya Burundi ya kuvikataza kutowa habari au udadisi kuhusu uchunguzi unaofanyika juu ya mauaji hayo ili ’’uchunguzi huo usipotoshwe’’. Makamo wa pili wa rais, Gervais Rufyikiri aliwaomba raia kushiriki wote kwa ujumla katika mpango wa kuboresha amani na usalama kwa kushirikiana na vyombo vya usalama, vyombo vya sheria na utawala.
Katika hutuba yake, mwaakilishi wa familia za wafiwa aliomba serekali ya Burundi ifuatilie kwa karibu uchunguzi huo unaofanyika ili waliohusika katika mauaji hayo ya Gatumba waadhibiwa vikali. Aliomba pia usalama mtaani humo Gatumba ulindwe ipasavyo. Mwaakilishi huyo wa familia za wafiwa alitolea wito serekali ya Burundi akiitaka ifuatilie kwa karibu hali ya majeruhi wanaolazwa hospitalini. Anasema 2 miongoni mwao itabidi wapelekwe kutibiwa ugenini.
Katika sherehe hizo wizara ya mshikamano wa kitaifa ilijiunga na familia za wafiwa na kila familia ilipewa zawadi au msaada ambao ni pamoja na mchele, maharage, chumvi, jembe vitenge, sabuni na vinginevyo kama ishara kua serekali ya Burundi inashikamana na raia hao wa Gatumba katika msiba huo.