Shirika la kimataifa la kutetea haki za wandishi wa habari, ”Reporters without Borders” linaomba Serekali ya Burundi ifutilie mbali hatua ya kuvikataza vyombo vya habari kutangaza habari kuhusu mauaji ya Gatumba kwa muda wa mwezi mzima.
Katika risala ambayo shirika hilo limemtumia Rais wa Jamhuri Pierre Nkurunziza na waziri wa habari Bii Concilie Nibigira, linabaini kua linasikitishwa na hatua hio ya kupiga marfuku katika kipindi cha mwezi mzima matangazo ya moja kwa moja au vipindi vya kisiasa kuhusu uchunguzi unaofanyika juu ya mauaji yaliyotekea hapo ijuma pili nyakati za saa mbii za usiku huko Gatumba.
Shirika hilo la kimataifa la kutetea haki za wandishi wa habari, ”Reporters without Borders” linawaomba viongozi wa Serekali ya Burundi wafutilie mbali hatua hio ya kuwakataza wanahabari ”kuchapisha, kutowa maelezo au udadisi kuhusu uchunguzi unaofanyika juu ya mauaji ya kikatili ya Gatumba”. Shirika hilo linasema uamzi huo wa serekali ya Burundi ni ”hatua kali kupitiliza”. Linabaini kua linaunga mkono hatua iliyochukuliwa na muungano wa maredio wa kutowa habari kuhusu swala tete la usalama unaozidi kuyumbishwa nchini Burundi.
Shirika hilo la kimataifa la kutetea haki za wandishi wa habari, ”Reporters without Borders”, linakiri kua mauaji ya kinyama yaliyoendeshwa huko Gatumba ni ya kutisha na yanaweza kuleta mvutano walakin ifahamike kua harakati za kuboresha amani haziwezi kamwe kwenda sambamba na ukiukwaji wa uhuru wa vyombo vya habari, linasema Shirika hilo. Badala ya hayo, kuna umuhimu kuhimizwe mazungumzo kati ya pande zote na raia wahakikishiwe haki yao ya kupata habari kuhusu yanayojiri nchini, linazidi kusema Shirika hilo la kimataifa la kutetea haki za wandishi wa habari ”Reporters without Borders”.