Serekali ya Burundi na vyombo vya habari havielewani kuhusu utangazaji habari zihusuzo mauaji ya raia wasiopunguwa 39 yaliyotokea huko Gatumba magharibi mwa mji wa Bujumbura hapo ijuma pili usiku katika shambulio lililoendeshwa na watu wenye kubebelea silaha na kuvalia sare za kijeshi na za polisi. Hasa kinachopigwa marfuku ni habari juu ya uchunguzi unaofanyika kuhusu mauaji hayo ya kikatili, na yote hayo ni kwa muda wa mwezi moja.
Kutoelewana huko kati ya Serekali ya Burundi na vyombo vya habari ni kufuatia maagizo ya Baraza Kuu la Usalama nchini Burundi kuhusu mauaji hayo. Maagizo yenyewe yalikua ni hasa kuwakataza wanaharakati wa haki za binadamu, wandishi habari na wanasiasa wasithubutu kutowa maelezo yahusuyo uchunguzi juu ya mauaji hayo. Hapa kulitolewa tahadhari kwa yeyote yule atakaekiuka au kwenda kinyume na amri hio.
Kilicho dhahiri ni kwamba taarifa ya waziri wa habari, Bii Concilie Nibigira ya kuvikataza vyombo vya habari vyote kwa ujumla visitangaze habari zihusuzo mauaji hayo hasa udadisi juu ya uchunguzi unaofanyika, ni kutokana na maagizo ya Baraza kuu hilo la usalama nchini Burundi.
Licha ya hayo vyombo vya habari vinavyobaini kua tangu mwezi mei kulimaliziwa maisha watu wasiopunguwa 250 pakiwemo mauaji ya Gatumba, havikutii amri hio ya waziri wa habari sababu bada tu ya taarifa ya Bii Concilie Nibigira kutolewa kama tahadhari akisema ni kutokana na « sababu za kiusalama », vyombo vya habari ikiwa ni pamoja na CCIB FM+, Bonesha FM, Isanganiro, RPA na Télévision Renaissance viliamua kujiunga na kufanya taarifa ya habari kwa pamoja. Redio Rema FM na Redio ya taifa, RTNB vilijiondowa kwenye muungano huo wa maredio.
Katika taarifa ya waziri wa habari, maredio yanatakiwa pia kwa kipindi hiki cha mwezi moja cha uchunguzi kuhusu mauaji ya Gatumba kutowaalika studioni wanasiasa na kuanza kudadisi moja kwa moja hali ya mambo wakati huu kunakoendeshwa uchunguzi huo walakin vyombo vya habari vyenyewe viliwaitisha marais wastaafu Domitien Ndayizeye, Pierre Buyoya na Sylvestre Ntibantunganya ili watowe mitazamo yao kuhusu hali inayojiri nchini Burundi. Viongozi hao wa zamani wa Buruni ambao wote ni maseneta walisisitiza umuhimu wa kukomesha mauaji na hasa kuanzisha mazungumzo ya kisiasa baina pande zinazohasimiana ili raia wasizidi kunyanyaswa na kuuwawa.
Viongozi wa maredio wanabaini kua la muhimu wakati huu ni kufuatisha sheria na nidhamu ya upashaji habari katika utendaji kazi na kusuta kidole bila kusita ukiukwaji wa haki za binadamu hasa kuwamalizia maisha raia.